
Ardhi ya Zulani EPS 1
Wanasema mapenzi ni upofu. Naye anasema kuwa upofu ulimpata pale alipopenda.
Lakini afanye nini? Alishapenda, na lililopangwa kuwa, limeshakuwa.
Huyu hapa, amekaa chumbani kwake kama ilivyo kawaida yake kila siku, akiandika tena waraka mwingine.
“Mimi ni Habil Hosny, kijana wa miaka ishirini na minane, mhitimu wa kitivo cha biashara mjini Kairo tangu miaka sita iliyopita.
Kijiji changu kinaitwa Al-Baho Frik, kilichopo katika jimbo la Dakahlia. Na leo hii, nimekataliwa kumuoa mpenzi wangu kwa mara ya nane, na kwa sababu ileile”.
Kisha akatazama ukutani. Akasimama na kuutundika waraka huo karibu na nyaraka nyingine saba, ambazo zilionekana wazi kuwa zilitundikwa nyakati tofauti za huko nyuma.
Waraka wa kwanza uliandikwa jina lake, umri wake, na kijiji chake, kisha
ukafuatiwa na maneno, Nimekataliwa kumuoa mpenzi wangu leo. Pembeni yake
kulikuwa na waraka wa pili ulioandikwa, Nimekataliwa kwa mara ya pili. Na wa
tatu, Nimekataliwa kwa mara ya tatu. Hivyo hivyo mpaka waraka wa saba.
Baada ya hapo, aliuegesha mgongo wake nyuma na kutazama juu. Kumbukumbu zake zikamrudisha miaka sita iliyopita, wakati alipokuwa akisoma mwaka wa mwisho chuo kikuu. Mipango ya Mungu ilimkutanisha na Mona, binti wa kijijini kwao.
Walikutana kwa bahati mbaya njiani wakitoka kijijini kuelekea chuo kikuu Kairo. Furaha yake iliongezeka alipojua kuwa binti huyo alikuwa akisoma chuo kilekile
alichokuwa akisoma yeye, akiwa mwaka wa kwanza. Tangu siku hiyo, mikutano yao iliongezeka, iwe kwa kupanga au kwa bahati mbaya tu.
Zinduko lilimjia alipovuta pumzi nzito na kutazama ule waraka mkubwa
alioutundika chini ya zile nyaraka nane uliosomeka “Nimekataliwa kwa sababu
ileile, Baba yake Mona ni mwendawazimu”.
Ikiwa Habil angesikia neno mwendawazimu, daima angemkumbuka baba yake Mona. Na hakua yeye pekee, bali watu wote wa kijiji walimjua kwa ubishi wake.
Tangu alipomaliza masomo yake na kuamua kwenda kumposa Mona, alishangazwa katika ziara yake ya kwanza kuona mzee huyo akimtazama kwa mshangao na kumuuliza:
– Unataka kumuoa Mona?
Habil alijibu:
– Ndiyo.
Mzee akamuuliza tena:
– Je, umefanya nini katika maisha yako?
Habil alibadilika sura, akahisi kuchanganyikiwa kwani hakutarajia swali hilo.
Alijibu kwa tahadhari:
– Nimefanya nini katika maisha yangu? Ukweli ni kwamba mimi ni mhitimu wa kitivo cha biashara chuo kikuu cha Kairo. Na kama unavyojua, wazazi wangu walifariki nikiwa mdogo, naishi na babu yangu. Nimesamehewa kwenda
jeshini, na kwa sasa natafuta kazi inayonifaa.
Baba yake Mona alimkatisha:
-Je, una utofauti gani na wengine mpaka nikuoze binti yangu?
Kisha mzee huyo alikataa posa hiyo.
Habil aliamini wakati huo kuwa sababu ya kukataliwa ni kukosa kazi maalum,
lakini alijiridhisha kuwa huenda haikuwa hivyo pale alipopata kazi na kwenda
tena kumposa Mona kwa mara ya pili, na kukumbana na swali lilelile. Umefanya
nini katika maisha yako? Una utofauti gani na wengine? Ni swali ambalo hakupata
jibu lake kamili mpaka mara ya nane alipokwenda tena. Alijitahidi kumweleza
jinsi anavyompenda binti yake, lakini mzee alimkatalia kwa dharau.
Siku hiyo, Habil alipandwa na hasira na kumjibu kwa sauti ya juu:
– Sijafanya chochote katika maisha yangu… Nifanye nini yaani? Unajua kwamba tulipigana vita mwaka sabini na tatu. Unaona hii ni sababu ya kunidhalilisha hivi? Sawa, unataka shujaa kwa binti yako. Niambie niwe shujaa vipi? Niende kupigana vita Iraki ndio ufurahi?
Mzee alimtazama, hasira zikionekana machoni pake, na kumjibu:
-Utamuowa na Mona kwa lazima…? Sikutaki na swala hilo sahau.
Kijiji kizima kilijua tabia za ajabu za mzee huyo. Alitaka kumuozesha binti yake
wa pekee kwa mtu wa kipekee. Mtu wa aina gani? Hakuna aliyejua. Kila mmoja
alijua mwisho wa binti huyo itakuwa ni kuzeekea nyumbani. Hata hivyo, Habil
hakukata tamaa. Hakukuwa na kingine akilini mwake isipokuwa kumfanya awe mtu wa kipekee, mtu anayestahili kumuoa Mona kama baba yake alivyotaka. Lakini nini hicho? Hakujua. Alibaki kumuomba Mungu amchukue baba mkwe huyo mtarajiwa.
Pamoja na kwamba Habil alikuwa ni kijana mchangamfu na mwenye uso wa tabasamu, mapenzi yake kwa Mona na kukataliwa mara kwa mara kulimvika joho la huzuni ambalo lilidumu usoni pake. Babu yake, mzee wa miaka karibu themanini, ambaye aliishi naye tangu wazazi wa Habil walipofariki, aliona huzuni hiyo kubwa.
Alimwendea na kumuuliza:
-Bado umekasirika? Ulipaswa uwe ushazoea sasa hivi.
Habil alijibu kwa uchungu;
-Siwezi kuvumilia kumuona akiwa wa mtu mwingine… Na sijui baba yake anataka nini. Hajui kama enzi za miujiza zimeshapita.
Babu alicheka kidogo akimtania:
-Basi huna budi kujizika kwenye handaki…
Macho ya Habil yaling’aa kana kwamba alikumbuka kitu. Handaki? Alisema:
-Ndiyo babu, unakumbuka nilipokuwa mdogo, nilipokuwa nikilia ulikuwa ukinisimulia hadithi ya lile handaki lililopo chini ya kijiji chetu? Kuwa uliteremka huko zaidi ya miaka hamsini iliyopita?
Babu alitabasamu:
-Ndiyo, nakumbuka. Unataka nikukumbushe enzi hizo?
Habil alicheka kwa mbali:
-Ndiyo, nisimulie tena kuhusu hilo handaki na mlivyoteremka.
Babu akavuta pumzi na kukumbuka:
-Yalikuwa ni masiku yaliyopita. Tulikuwa vijana wanne watukutu. Tulisikia hadithi nyingi kuhusu hazina iliyopo kwenye handaki linalopita chini ya kijiji chetu… Kwamba zamani lilikuwa ghala kubwa la matajiri wakati wa vita. Kila mtu alijua kuwa lile handaki lipo kweli, lakini hakuna aliyethubutu kuteremka kwa sababu liliaminika kuwa limekaliwa na majini na mizimu… Wale wazee walituonya, lakini sisi tulikaidi.
Babu aliendelea:
-Tulijua mlango wa handaki hilo upo kwenye nyumba moja iliyotelekezwa kijijini. Kulikuwa na jiwe kubwa mlangoni. Siku moja usiku, tulimtanguliza Mungu na kuelekea kwenye nyumba hiyo kwa siri. Tulifanikiwa kulisogeza lile jiwe na tukaanza kuteremka mmoja baada ya mwingine. Kila mmoja wetu alikuwa na taa ya mafuta… Baada ya kuteremka ngazi ndefu, tulijikuta kwenye njia ya chini kwa chini. Tulitembea hatua kadhaa mpaka tukahisi hatuwezi kupumua vizuri. Ghafla, taa zote zilizimika kwa wakati mmoja… Mmoja wetu akapiga kelele, Jini! Tulitimua mbio, kila mtu akishika njia yake kurudi nje. Tangu siku hiyo hakuna aliyejaribu tena kuteremka huko.
Habil alicheka:
-Ni kumbukumbu nzuri. Lakini mlishindwa kuingia vizuri, afadhali
mliokoa maisha yenu.
Babu aliukunja uso wake kwa mzaha:
-Usimwambie mtu hadithi hii ya uoga wetu.
Baadaye, Habil alirudi chumbani kwake… Alijaribu kulala lakini usingizi
Ulimruka.
Alifikiria sana yale aliyoambiwa na babu yake… Alijua aliyosikia yalikuwa kama hadithi za kufikirika, lakini handaki lilikuwepo kweli, na babu yake hakuwa muongo kamwe.
Ghafla alitazama kile kipande cha karatasi alichoandika sababu ya kukataliwa. Baba yake anataka mtu wa kipekee, mtu atakayeridhisha wazimu wake. Alijisemea moyoni mwake kuwa Mona hatoolewa na mtu mwingine ila yeye. Sauti yake ikapanda..
“Kuna ubaya gani nikishuka kwenye lile handaki? Tuseme kuna hazina kweli huko chini?”
Alijisemea mwenyewe kana kwamba anashawishi nafsi nyingine ndani yake. “Ndiyo, hili ndio suluhisho.”
Akaendelea kujisemea..:
“Ukiwa muoga, humstahili Mona. Unaridhika na maisha haya? Mhitimu wa biashara unafanya kazi kwenye ghala la madawa? Unaishi na babu yako maisha ya kawaida mno. Ukipata hazina hiyo, utakuwa mtu maarufu zaidi kijijini, labda nchini Misri nzima… Na hata usipoipata, inatosha kuonyesha kuwa ulijaribu.”
***
Aliruka kutoka kitandani… Akatoa picha ya Mona Akaitazama picha ile na kusema
kwa sauti ya dhamira thabiti…
“Nitateremka kwenye lile handaki. Nitateremka hata iweje. Na ikiwa baba yako ni mwendawazimu, basi mimi wakati mwingine ninakuwa wazimu wenyewe.”
Habil alidhani anajiongelesha mwenyewe. Hakujua kuwa babu yake alikuwa
amesimama nje ya mlango wa chumba hicho akisikiliza kila neno. Kinyume na
matarajio, uso wa babu huyo hakuonyesha mshtuko. Kusikia kuwa mjukuu wake
anataka kuteremka kwenye lile handaki hakukuwa jambo geni sana kwake, bali
kulionekana kama tukio ambalo alilitegemea litokee siku moja. Babu alisimama
kimya hadi sauti ya Habil ilipokata, na taa ya chumba kuzimwa. Utulivu ukitawala…ukivunjwa tu na sauti ya kupumua kwa mjukuu wake aliyekuwa amelala.
Kisha babu aliondoka akitegemea fimbo yake hadi chumbani kwake. Aliketi kimya
kitandani kwa dakika kadhaa. Akasogeza sanduku dogo la mbao lilioonekana la kale sana… Akalifungua, akatoa albamu ya zamani ya picha iliyojaa vumbi.
Aliipangusa vumbi na kuanza kupitia kurasa zake, picha baada ya picha, hadi aliposimama kwa muda mrefu kutazama picha moja. Machozi yalimlenga…
Siku iliyofuata, wote waliamka mapema kama kawaida yao. Habil alikuwa na kazi
yake ya asubuhi, na babu yake hakuwa na desturi ya kulala baada ya sala ya
alfajiri, akiendelea kusoma kitabu cha Mwenyezi Mungu mpaka Habil aamke, wapate kifungua kinywa pamoja. Katikati ya ukimya wa asubuhi, Habil alimwangalia babu yake na kuamua kusema…
“Abdu..”
ndivyo alivyopenda kumwita babu yake.
-Unaweza kuishi peke yako?
Babu alimtazama akijifanya hajaelewa..
-Unataka kusafiri au vipi?
Habil alinyamaza, kisha akamwangalia tena..
-Nikisafiri kwa muda mfupi, utaweza kuishi peke yako?
Aliendelea kujieleza..
-Najua maneno yangu yanakushtua, lakini nimeamua kuondoka kijijini kwa muda. Na nakuapia nitarudi haraka iwezekanavyo.. Sitakuacha kwa muda mrefu. Najisikia kwenda mahali nipate kujitafuta. Unajua mjukuu wako, mhitimu wa chuo, anafanya kazi gani..? Kazi ya kubeba mizigo kwenye ghala la madawa… Beba boksi hili weka hapa, chukua lile weka kule. Nataka mabadiliko.
Kisha Habil alisimama ili aondoke..
-Nitasafiri, lakini si kwa muda mrefu.
Alipofika mlangoni, sauti ya babu yake ilimsimamisha..
-Kwa nini unadanganya Habil? Kwa nini hutaki kuniambia ukweli kwamba unataka kuteremka kwenye lile handaki?
Maneno yale yalishuka kama radi kwa Habil. Alidhani babu yake angechanganyikiwa au kumwita mwendawazimu, lakini hakujua babu yake aligunduaje. Alimtazama kwa wasiwasi..
-Handaki? Umejuaje? Ninamaanisha handaki gani? Maneno gani haya ya
upuuzi?
Babu alimjibu kwa utulivu..
-Nilijua tangu zamani sana. Kaa chini.
Babu akamuuliza kwa umakini..
-Unataka kuteremka kwenye handaki kwa nini?
Habil alijaribu kupunguza uzito wa mazungumzo..
-Kwa nini umeshikilia stori za handaki? Nimekwambia nitasafiri.
Babu alirudia swali lake bila kubadilisha sauti..
-Habil, unataka kuteremka kwenye handaki kwa nini?
Habil alishusha pumzi ndefu na kukubali..
-Nataka niteremke ili nimthibitishie Mona na baba yake kuwa mimi ni shujaa. Kuwa nina utofauti na wengine.
Babu aliuliza kwa ufupi..
-Basi?
Habil alijibu..
-Ndiyo, basi. Na nani anajua, labda ninaweza kupata ile hazina ambayo nyinyi mlishindwa kuipata mlipoteremka zamani.
Babu alimwangalia kwa macho makali ambayo Habil hajawahi kuyaona..
-Na kama Mona akiolewa na mtu mwingine, je, bado utateremka kwenye lile handaki au la?
Habil alikaa kimya..,
Babu aliendelea..
-Sijawahi kuamini kuwa unataka kuteremka kwa ajili ya Mona… Wewe unataka kuteremka kwa sababu zilezile zilizonifanya niteremke mimi.., na alizoteremka baba yako…
-Ni damu inayotiririka kwenye mishipa yetu. Damu yangu, yako, na ya baba yako. Ni kiu yetu ya kutafuta yasiyojulikana.. Ni kiu yetu ya uasi dhidi ya maisha ya kawaida. Ni kiu yetu ya kugundua mapya.. Ni kiu yetu ya utofauti.
Babu alishusha sauti yake..
-Ulipokuwa mdogo ukiwa unalia, nilikuwa nikikusimulia hadithi ya lile handaki ili tu kukubembeleza.., lakini nilijua fika kuwa itafika siku utakua, na nitakusimulia tena.., na damu yako itachemka ndani yako.. Lakini unajua kwa nini baba yake Mona amekukataa kila mara..?
-Unajua kwa nini ulipofika jana ukihisi hamu ya kuwa shujaa ilikujia ghafla? Ni hisia ileile iliyomjia baba yako siku aliponiambia kuhusu handaki hili. Tofauti ni kwamba mimi nilijua tangu mwanzo kuwa unataka kuteremka.. Yeye aliamua ghafla.
Habil alimkatisha kwa mshtuko mkubwa..
-Baba yangu aliteremka kwenye lile handaki?!
Babu alijibu kwa sauti iliyojaa majonzi..
-Sio baba yako pekee.. Baba yako na mama yako wote.. Watu walidhani wamekwenda kwenye safari fupi na wangerejea.. Ndio maana walikuacha ukiwa na miaka miwili.
-Lakini siku zikawa miezi, miezi ikawa miaka. Kijiji kizima kikajua wamekufa kwenye ajali, na kila mtu alimshukuru Mungu kwamba hukuwa nao, na uliokoka. Lakini ukweli ni kwamba, waliteremka kwenye lile handaki.
Babu alihema na kuongeza..
-Sijawahi kujilaumu kwa hilo. Nilijisemea moyoni mwangu kuwa na mimi nilishateremka na nilinusurika… Tofauti ni kwamba wao hawakunururika… Kwa hivyo siwezi kukasirika ukitaka kuteremka. Hata kama najua uamuzi wako huu unaweza kunitenga na wewe milele.. Lakini unapaswa kuwa na uhakika kwamba unateremka kwa ajili yako mwenyewe. Sio kwa udanganyifu unouweka kichwani kwako kuwa unafanya hivi kwa ajili ya Mona. Ikiwa utaamua, niambie.
-Kwa sababu bado nina maneno mengi sana ya kukuambia kuhusu handaki la Furik.. Kuna mtu mwingine atakuambia mengi.
Baada ya mazungumzo hayo mazito, Habil hakuenda kazini kama kawaida yake.
Badala yake alielekea kumwona Mona baada ya kumpigia simu na kumwomba waonane kwenye eneo ndani ya chuo kikuu cha Mansoura, sehemu ambayo walizoea kukutana.
Njiani, hakuweza kuacha kufikiria maneno ya babu yake.. Picha ya wazazi wake
alioambiwa wamepotea kwenye handaki ilimzunguka akilini. Hakuwahi kujua sura zao isipokuwa kwa maelezo ya jamaa, au ile picha moja pekee aliyowahi kuiona. Je,
anafanya haya kwa ajili ya mapenzi ya Mona, au ni kwa ajili ya kutafuta ukweli
wa familia yake?
***
Alipofika kwenye eneo la ahadi.., alimkuta Mona anamsubiri. Alikuwa amevaa vazi
lile la heshima, lenye rangi nyeusi.. Rangi ambayo Habil daima alimwambia inamletea mkosi pindi anapokutana naye… Habil alimtazama kwa tabasamu, lakini
Mona hakutabasamu kama ilivyo kawaida yake.
Mona alisema..
-Ninasikitika sana kwamba baba amekufanyia vile kwa mara ya nane.
Habil alicheka kwa mbali kujifariji..
-Hapana, nimeshazoea.. Nimekuwa kituko cha kijiji sasa hivi. Watu wanasema nimevunja rekodi ya kukataliwa kwako.., kwamba nastahili kuingia kwenye kitabu cha rekodi za dunia cha Guinness. Lakini haikusaidia.
Mona aliendelea huku sauti yake ikitetemeka..
-Nilikuwa nikifikiria sana. Daktari mmoja amekuja kuniposa. Na cha kushangaza, baba amekubali…
Habil alishtuka..
Nini? Amekubali?!
Mona alianza kutokwa na machozi huku akisema..
-Ndiyo… amekubali na anashikilia niolewe naye. Nilijaribu kuongea naye kuhusu mapenzi yangu kwako… akanipiga kofi usoni… Akasema yeye anajua zaidi kilicho chema kwangu.. Kuwa mustakabali wangu una uhakika kwa daktari huyu, na kwamba kwako nitateseka tu.
Habil alibaki kimya.. Akili yake iliganda..Je, haya ni kweli? Huyu mzee
mwendawazimu anataka nini hasa? Ikiwa alitaka kumuoza binti yake kwa mtu tofauti na shujaa, kwa nini kakubali daktari wa kawaida? Na kwa nini Mona hakupinga uamuzi huo..? Je, aliogopa kuzeeka nyumbani? Maswali haya yalizunguka akilini mwake wakati Mona akiendelea kuongea, na mwishowe akamuomba waagane ili asichelewe kurudi nyumbani, kana kwamba alikuwa anaikimbia mikutano yao.
Habil alitabasamu kwa kejeli na kumpungia mkono aondoke bila kusema neno..
Ilikuwa ni mara ya kwanza kwake kumwacha Mona aondoke peke yake. Alibaki amekaa, akimtazama akipotea kwa mbali, akihisi kukabwa kooni na maumivu makali.. Hii ilikuwa mara ya kwanza kuhisi hisia za kushindwa kwa kiasi hiki. Katika mara zote nane alizokataliwa na baba yake, daima alikuwa na tumaini. Hata kama angekataliwa mara mia.., alijua angeweza kujaribu tena. Lakini sasa, tumaini
limekufa.
Akiwa anatembea kurudi kijijini kwake, kichwa chake kilikuwa chini.. Akijihisi
mnyonge. Hakutaka kuongea na mtu yeyote mpaka alipofika chumbani kwake.
Akatazama zile nyaraka nane alizozitundika ukutani.. Nyaraka zilizobeba aibu na
kukataliwa kwake..
Akazitazama kwa dharau, akacheka kicheko kilichojaa wazimu, na kuanza kuzichana zote.. Akakaa sakafuni, akiweka kichwa chake kati ya mikono yake, na kupotea kwenye mawazo.. Kisha, alinyanyuka ghafla na kuelekea chumbani kwa babu yake. Alimkuta babu yake ndiyo kwanza anamaliza kusali.
Habil akamuuliza moja kwa moja..
-Uliniaambia kuna mtu ana maneno mengi kuhusu lile handaki.
Babu alimjibu kwa utulivu..
-Je, umeshakata shauri?
Habil alijibu..
-Ndiyo. Nataka kuteremka kwenye lile handaki.Babu aliuliza..
-Kwa ajili ya Mona?
Habil alijaribu kuzuia hisia zake na kusema..
-Mona ameshaondoka mikononi mwangu..Na nimeshaacha kazi yangu. Lazima niteremke… Lazima nipate walau jambo moja maishani mwangu niliweze kujivunia baadaye.. nikiwasimulia watoto wangu.. Nataka kuhisi japo mara moja kuwa mimi ni shujaa mbele ya nafsi yangu. Hisia ya kushindwa inaniua.
Babu alimuuliza..
-Huogopi kutokurudi kama walivyofanya wazazi wako?
Habil akajibu..
-Niamini, hofu yangu pekee ilikuwa kukuacha wewe peke yako… Lakini kwa kuwa unaniunga mkono, sina hofu yoyote moyoni mwangu.. Sidhani kama nitakutana na jini ambalo linatisha zaidi kuliko wanadamu. Nimeamua kweli kuteremka.. Na ukiwa sawa na ulichokisema.., kuwa Mona siyo sababu yangu, basi upo sahihi.
-Baada ya Mona kupotea.., hamu yangu ya kuteremka imeongezeka mara dufu. Huenda nikapata ile hazina ndani ya lile handaki ikanisaidia kusahau matusi na unyonge wa miaka sita mfululizo.
Habil alimuuliza tena babu yake..
-Yuko wapi huyo mtu, na naweza kumpata wapi?
Babu alitabasamu..
-Tulia.. Yuko hapa na amesikia mazungumzo yetu yote. Pengine naye ameshajiridhisha sasa kuwa unataka kweli kuteremka.
Habil alishangaa.. Hakuelewa nini kinaendelea. Lakini wakati huo huo, mlango
ulifunguliwa na mzee mmoja akiwa ameinama, na umri unaokaribiana na babu yake, akaingia chumbani.
Babu yake alimwangalia Habil na kusema..
-Nikupe heshima kumtambulisha kwa Mwendawazimu wa Handaki.. Nina uhakika unamjua… Je, ni nani hasa huyu anayeitwa “Mwendawazimu wa Handaki”? Ni siri gani nzito iliyowameza wazazi wa Habil miaka yote hiyo bila kurudi? Na je, Habil anapiga hatua ya kuelekea kwenye hazina ya ushujaa, au ndio anajiingiza kichwakichwa kwenye mtego hatari utakaomgharimu maisha yake?
Gizani kuna mengi yaliyojificha… na milango ya handaki iko tayari kufunguka.
USIKOSE SEHEMU YA PILI! Mambo yanazidi kuchacha, siri zinaanza kufichuka, na safari ya kuelekea kusikojulikana ndio inaanza rasmi.

sehemu ya pili iko wapi?
hamna shida kiongozi itakuja mda si mrefu na utalipia kiasi kidogo tu kusoma
Unyama sana